Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ASISITIZA OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UFANISI.

Imewekwa: 30 March, 2026
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ASISITIZA OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UFANISI.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kufanya kazi kwa weledi na ufanisi ili kufikia malengo ya ofisi.

 

Mhe. Hamza amesema hayo alipofungua kikao cha kwanza cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria jijini Dar es Salaam.

 

"Niwaombe muendelee kutekeleza majukumu ya ofisi hii kwa weledi na ufanisi ili kufikia malengo ya ofisi na nina imani kubwa na utendaji kazi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, " amesema Mhe. Hamza

 

Mhe. Hamza ameendelea kwa kuwataka watumishi wa kuzingatia kanuni na sheria za utumishi wa umma ili tusiathiri utendaji kazi wa Serikali.

 

"Utumishi wa umma unaongozwa na sheria pamoja na kanuni, hivyo natoa rai kwa watumishi wote tuzingatie miongozo ya utumishi wa umma ili tusiathiri utendaji kazi wa Serikali," ameongeza Mhe. Hamza

 

Mhe. Hamza ameitaka ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kuboresha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kufanya kazi kwa ufanisi.

 

"Naomba nisisitize matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi na kutoa kazi zenye ufanisi kwa matumizi ya serikali na jamii kwa ujumla," ameeleza Mhe. Hamza.

 

Akitoa hotuba yake, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole, Ofisi imewekeza nguvu kubwa kwenye mifumo ya TEHEMA ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi.

 

"Katika kuendelea kuimarisha ya utekelezaji wa uandishi wa sheria tumeamua kuweka nguvu kubwa kwenye mifumo ya tehama kwa kuanzisha e-drafting e-translation na e-revision na kwa usaidizi wako Mwanasheria Mkuu wa Serikali tutaweza kufanikisha hili.

 

Bw. Onorius ameendelea kwa kusema kuwa Baraza hili la Wafanyakazi ni mafanikio makubwa kwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.

 

"Baraza hili kwetu ni mafanikio makubwa kwani ni sehemu ya wafanyakazi kujadili masuala ya kiutumishi na kupitia baraza hili tutajenga utaratibu wa mawasiliano ya wazi," ameeleza Bw. Onorius.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameipongeza ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kikao cha kwanza cha baraza.

 

"Ofisi hii ni wadau wetu muhimu sana hivyo niwapongeze kwa kikao hiki cha kwanza cha baraza kwani baraza ni kikao muhimu kinachoonganisha wajumbe na menejimenti ili kutatua changamoto za watumishi," amesema Bw. Sylvester