Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ina jukumu la msingi la kubadili sera kuwa sheria ambazo zinasaidia upatikanaji wa haki, usawa na maendeleo. Watumishi wetu ambao ni waandishi wa sheria, mawakili wa serikali, warekebu wa sheria, makatibu sheria na watumishi wengine ni msingi wa kazi zetu, wakileta utaalamu, uadilifu na kujitolea katika kila jukumu la kutunga sheria. Tangu ilipoanzishwa kama sehemu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, OCPD imeendelea kutekeleza maono ya dira yake kuwa kitovu cha ubora katika uandishi wa sheria. Jukumu letu huanza pale ambapo hitaji la sheria linapotambuliwa na tunaendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uandishi wa sheria, vikao vya Bunge na hata baada ya sheria kupitishwa, tunahakikisha kwamba sheria zilizotungwa zinakidhi kwa ufanisi. Huduma zetu zinalenga kutoa sheria bora, zinazopatikana kwa urahisi na kwa usahihi kwa ajili ya kujenga msingi imara kwa maendeleo endelevu. Zaidi ya uandishi wa sheria, tunashirikiana kwa karibu na Bunge, Mahakama, taasisi za serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa sheria zinapatikana kwa lugha rahisi ili kukidhi dhamira yetu ya upatikanaji wa sheria bora kwa kila mtu. OCPD pia imedhamiria kukuza ushirikiano utakaochangia uthabiti wa kiuchumi, ukuaji wa maendeleo na haki za binadamu na kujenga msingi endelevu.