Neno kutoka kwa Mwandishi Mkuu wa Sheria
.
Kutoka kwa Mwandishi Mkuu wa Sheria
Kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), nina furaha kuwakaribisha kwenye tovuti rasmi ya OCPD.
OCPD ni kitovu cha utaalamu wa uandishi wa sheria nchini. Majukumu yetu yanajumuisha uandishi wa sheria na uchakataji wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria, uandaaji na utangazaji wa tafsiri rasmi ya sheria, urekebu wa sheria pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali, Bunge, Mahakama na wadau wengine. Tunahakikisha kwamba sheria zote zinazopitia hatua za uandishi, tafsiri, urekebu au marekebisho zinazingatia viwango vya kitaifa, kikatiba na kimataifa, na zinakidhi mahitaji ya jamii.
Tovuti hii imeundwa ili kutoa taarifa, kuelimisha na kuwezesha utaratibu wa ushirikiano na mrejesho kutoka kwa wadau mbalimbali katika masuala ya kisheria hususan katika mchakato wa uandishi wa sheria na huduma nyingine za kisheria zinazotolewa na OCPD.
Tunaamini kwamba tovuti hii itawezesha wadau kupata kwa urahisi taarifa muhimu zinazohusiana na shughuli za OCPD zikijumuisha nyaraka za kisheria, taarifa za shughuli za OCPD, pamoja na mambo mengine muhimu kama picha mjongeo na mnato zinazoonesha majukumu yetu. Aidha, tovuti hii itatoa fursa ya ushirikishwaji wa wadau kwa kukaribisha mrejesho na maoni, kwa lengo la kuboresha huduma zetu.
Tunatoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wabunge, taasisi za Serikali, Mahakama, Wizara, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla, kutembelea tovuti hii na mitandao yetu ya kijamii mara kwa mara ili kujifunza zaidi kuhusu shughuli za OCPD.
Asanteni kwa kuendelea kuiunga mkono OCPD. Tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu kuendelea kutumia taarifa zilizopo katika tovuti yetu. Tunaahidi kuendelea kutoa huduma kwa uweledi ili kukidhi matarajio ya Watanzania wote.
Karibuni sana!
Onorius J. Njole
Mwandishi Mkuu wa Sheria