Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

Historia ya Taasisi

 

HISTORIA YA TAASISI

Historia ya OCPD inaelezwa vyema na mabadiliko yaliyofanyika katika nyakati tofauti yanayogusa muundo wa kitaasisi na mfumo wa utekelezaji wa majukumu ya uandishi wa sheria yaliyolenga kuendana na mahitaji ya wakati husika. Licha ya uchache wa waandishi wa sheria na ufinyu wa mafunzo rasmi, katika kipindi chote cha mageuzi, menejimenti na watumishi wote wamekuwa na mchango muhimu katika kufanikisha mageuzi hayo hususani mabadiliko ya mfumo wa kisheria kutoka sheria za kikoloni kwenda mfumo wa sasa wa sheria za Bunge.

Kabla ya kuwa OCPD, Ofisi hii ilianza kama Kurugenzi ya Uandishi wa Sheria na baadaye ikabadilika kuwa Divisheni ya Uandishi wa Sheria kufuatia mabadiliko ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ikiwa kama Divisheni, imeendelea kutoa mchango muhimu katika uandishi wa sheria na hivyo kuchangia ukuaji wa tasnia ya sheria, kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini.

Kwa kutambua ukubwa na umuhimu wa majukumu ya msingi ya Divisheni, mwaka 2023, Bunge, kupitia Sheria Na. 11 ya 2023, lilianzisha OCPD. Sheria hii imeongeza kifungu cha 7A katika Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268, ambacho pamoja na kuanzisha OCPD, kinaipa uhuru Ofisi hii katika kutekeleza majukumu ya kiutendaji na kibajeti. Mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha ufanisi na utekelezaji wa majukumu ya uandishi wa sheria ili kuendana na mahitaji ya kisheria ya nchi.

Majukumu ya OCPD yanagusa maeneo mbalimbali ya shughuli za Serikali. Majukumu hayo yanajumuisha kuzishauri wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali na taasisi nyingine za Serikali katika mchakato wa uandishi wa sheria, ufasiri wa sheria, urekebu wa sheria, uandaaji wa mapendekezo ya sheria na hati za kisheria. Pamoja na majukumu haya, OCPD pia ina wajibu wa kuhakikisha kuwa miswada ya sheria za Serikali inaandaliwa kwa kuzingatia maamuzi ya Baraza la Mawaziri. Halikadhalika, OCPD ina jukumu la kuhakikisha kuwa miswada ya Serikali inaandaliwa kwa kuzingatia kalenda ya utungaji wa sheria. Ofisi hii pia ina jukumu la kuandaa maazimio kwa ajili ya kuridhiwa na Bunge na kushauri kuhusu uwasilishaji wa sheria za Muungano katika Baraza la Wawakilishi. Aidha, majukumu mengine ya OCPD ni kufanya utafiti na kuanzisha mafunzo ya uandishi wa sheria sambamba na kuimarisha mfumo wa kisheria ili kuwezesha upatikanaji wa haki na huduma nyingine katika sekta mbalimbali na umma kwa ujumla.