Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗢𝗖𝗣𝗗 𝗬𝗔𝗪𝗔𝗡𝗢𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜, 𝗬𝗔𝗪𝗘𝗞𝗔 𝗠𝗦𝗜𝗡𝗚𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗚𝗘𝗨𝗭𝗜 𝗬𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔

Imewekwa: 30 March, 2026
𝗢𝗖𝗣𝗗 𝗬𝗔𝗪𝗔𝗡𝗢𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜, 𝗬𝗔𝗪𝗘𝗞𝗔 𝗠𝗦𝗜𝗡𝗚𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗚𝗘𝗨𝗭𝗜 𝗬𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu majukumu, mwelekeo wa kimkakati na maandalizi ya taasisi katika kukabiliana na mabadiliko ya kisheria na kiteknolojia kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi na vyombo vya habari, pamoja na kuhakikisha taarifa zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya kisheria zinawasilishwa kwa umma kwa usahihi na weledi. Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Urekebu, Utafiti na Mafunzo, Bi. Rehema Katuga, amesema kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa maelekezo ya kutambua sheria zinazohitaji marekebisho ili ziendane na mahitaji ya sasa na mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya 2050. "Tumeshaanza zoezi la kutambua sheria zilizopitwa na wakati kwa lengo la kufanyiwa urekebu ili ziendane na wakati tuliopo kwa sasa," amesema Bi. Rehema. Bi. Rehema ameendelea kwa kueleza kuwa OCPD ipo tayari kushirikiana na Mawizara pamoja na Mataasisi kutungua na kufanyia Urekebu Sheria mbalimbali ambazo zitachochea katika utekelezaji wa Dira 2050. “OCPD kwa kuhakikisha tupo tayari kwa utekelezaji wa dira, tumeanza kuandaa watalamu kwenye masuala ya AI na teknolojia mpaka 2050 sehemu kubwa ya biashara itakua ikiendeshwa kidigitali hivyo lazima kuwe na maandalizi kwenye masuala ya kisheria ili Wizara ikituletea hitaji tunatakiwa kuwa tayari.” Ameeleza Bi. Rehema. "OCPD ipo tayari kushirikiana na sekta za kimkakati ikiwa ni pamoja na biashara, sekta binafsi na umma ambazo zinahitaji maboresho au ushauri wa kitaalamu wa kisheria ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi," ameongeza Bi. Rehema Mafunzo hayo yameweka msingi wa uelewa mpana kuhusu nafasi ya Ofisi katika mageuzi ya sheria na maandalizi ya nchi kuelekea uchumi wa kidijitali. Ofisi imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mfumo wa kisheria unakuwa jumuishi na unaoendana na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.