KAMATI YA BUNGE YARIDHIA BAJETI YA OCPD
KAMATI YA BUNGE YARIDHIA BAJETI YA OCPD
Imewekwa: 31 March, 2026
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imepata ridhaa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mhe. Edwin Enosy Swalle, kuipitisha Randama ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 katika kikao kilichofanyika Machi 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma. Randama hiyo imebeba vipaumbele vya kimkakati vinavyolenga kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za Ofisi, kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA kupitia mifumo ya kidijitali itakayorahisisha michakato ya uandishi wa sheria na usimamizi wa nyaraka za kisheria, kuandaa miswada ya sheria yenye ubora ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sambamba na kutoa toleo la urekebu wa sheria ndogo kwa mwaka 2027 na toleo la ufasiri wa sheria ndogo ili kuboresha upatikanaji na uelewa wa sheria hizo kwa wadau. Sambamba na hilo, Ofisi itaendelea kuimarisha ubora wa miswada ya sheria na nyaraka nyingine za kisheria zinazochapishwa katika Gazeti la Serikali ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kitaaluma na kisheria, lakini pia juhudi zitaelekezwa katika kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo endelevu, kwa lengo la kuongeza weledi, ubunifu na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi. Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara na taasisi zake, Eliakim Maswi Katibu Mkuu wa Wizara aliishukuru Kamati kwa ushauri na miongozo yake ambayo imechangia katika kuimarisha shughuli za sekta ya sheria Nchini. Katibu Mkuu pia aliishukuru Serikali kwa kuipatia OCPD fedha kwa ajili ya urekebu na ufasiri wa sheria ndogo ili kuimarisha uelewa wa sheria kwa wananchi. Wakichangia makadirio hayo ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, wajumbe wa Kamati, wameipongeza Serikali kwa kuendela kuimarisha sekta ya sheria. Mhe Enos Swalle alieleza umuhimu wa sheria za nchi kusomana ili kuwezesha Serikali kufikia malengo ya Dira 2050. Kupitishwa kwa Randama hiyo ni hatua muhimu kuelekea maandalizi ya mwisho ya Hotuba ya Bajeti itakayowasilishwa rasmi katika Mkutano wa Bunge la Bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
