Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

OCPD YASHIRIKI MKUTANO WA 70 WA TUME YA HADHI YA WANAWAKE DUNIANI (CSW70)

Imewekwa: 16 April, 2026
OCPD YASHIRIKI MKUTANO WA 70 WA TUME YA HADHI YA WANAWAKE DUNIANI (CSW70)
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali (OCPD) imeshiriki katika Mkutano wa 70 wa Tume ya Hadhi ya Wanawake Duniani (CSW70) uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 19 Machi 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, ambapo ushiriki huo umelenga kufuatilia na kuchangia mijadala ya kimataifa kuhusu kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana kupitia mifumo ya sheria jumuishi, yenye usawa na isiyobagua. Mkutano huu ambao OCPD imewakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Ufasiri wa Sheria, Bi. Frida Mwera, umekuwa jukwaa muhimu la kimataifa lililolenga kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha usawa wa kijinsia na upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana kupitia mifumo ya sheria jumuishi. Katika kipindi cha mkutano, Ofisi imefuatilia kwa karibu mijadala ya nchi wanachama, mikutano ya ngazi ya juu ikiwemo Ministerial Round Table iliyowakutanisha mawaziri na viongozi wa mataifa mashirika pamoja na matukio ya pembeni yaliyolenga kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyowakabili wanawake na wasichana, kuimarisha huduma za msaada wa kisheria, na matumizi ya teknolojia katika kuboresha upatikanaji wa haki.   Aidha, maazimio ya pamoja (Agreed Conclusions) yaliyopitishwa katika mkutano huo yametoa mwelekeo wa kimataifa kuhusu hatua za kuchukua ili kuhakikisha mifumo ya sheria inalinda na kukuza haki za wanawake na wasichana. Kupitia maazimio hayo, Ofisi imejipanga kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia, kuondoa vipengele vinavyobagua, na kuhakikisha sheria zinazoandaliwa zinazingatia viwango vya kimataifa vinavyolenga kukuza haki na ustawi wa wanawake na wasichana.   Vilevile, Ofisi imejifunza umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa utungaji wa sheria ili kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kisheria yanakuwa na ufanisi na uendelevu. Mbinu hii inahusisha kufanya mashauriano ya kina na wahusika wanaoathiriwa na sheria husika, kwa lengo la kuelewa kwa undani mazingira yao ya kijamii na kiuchumi pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo. Uelewa huo huchangia katika kubuni sera na hatua za kisheria zinazoendana na uhalisia wa maisha yao.   “Kwa mfano, katika jitihada za kutokomeza vitendo vya ukeketaji wa wanawake, imebainika kuwa hatua za kisheria pekee za kuzuia vitendo hivyo haziwezi kufikia matokeo endelevu endapo hazitaambatana na mikakati ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa wahusika wanaotegemea shughuli hizo kama chanzo cha kipato. Hivyo, utoaji wa elimu na uanzishaji wa njia mbadala za kujipatia kipato ni nyenzo muhimu zinazosaidia utekelezaji madhubuti wa sheria na kukubalika kwake katika jamii.” Amesema Bi. Mwera.   Ushiriki huu umeiwezesha Ofisi kubaini maeneo ya kipaumbele ya kuzingatiwa katika Utungaji wa Sheria ili kuondoa vipengele vinavyoweza kubagua na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana.   Sambamba na hilo, Ofisi imeshiriki katika matukio ya pembeni (side events) yaliyotoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano na taasisi za kimataifa katika masuala ya utungaji wa sheria unaozingatia jinsia, ambapo maarifa na uzoefu uliopatikana katika mkutano huo utatumika kuimarisha mchakato wa uandishi wa sheria nchini, hivyo kuhakikisha mifumo ya sheria inaendelea kuwa jumuishi na inayokidhi viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.