MUSWADA WA SHERIA YA MIKOPO KWA DHAMANA YA MALI ZINAZOHAMISHIKA WA MWAKA 2026 KUONGEZA UPATIKANAJI WA MIKOPO NA KUCHOCHEA UCHUMI
Serikali imewasilisha Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana ya Mali Zinazohamishika wa mwaka 2026, unaolenga kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima na wajasiriamali ambao mara nyingi hukosa dhamana za mali zisizohamishika kama ardhi au nyumba.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa muswada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria, Bw. Nicodemus Chuwa, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha mfumo wa kifedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi. Amesema muswada huo utawezesha matumizi ya mali zinazohamishika kama dhamana ya mikopo katika taasisi za kifedha.
“Muswada wa kisheria utawezesha wananchi kutumia mali zinazohamishika kama dhamana ya mikopo na hivyo kupanua fursa za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara na shughuli za uzalishaji,” amesema Bw. Chuwa.
Kwa mujibu wa muswada huo, mali zinazohamishika ni zile zinazoweza kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuharibu asili yake. Mali hizo zinajumuisha magari, mitambo, samani, vifaa vya kielektroniki, mifugo, mazao ya kilimo, hisa pamoja na mali nyingine zitakazotambuliwa rasmi kupitia notisi itakayotangazwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha, muswada unapendekeza kuanzishwa kwa Masijala Maalumu ya Usajili wa Dhamana za Mali Zinazohamishika itakayokuwa chini ya Benki Kuu ya Tanzania. Mfumo huu utawezesha usajili na uhifadhi wa taarifa za dhamana, kuthibitisha umiliki wa mali, pamoja na kuondoa hatari ya mali moja kutumika kama dhamana mara mbili au zaidi bila taarifa rasmi.
Bw. Chuwa ameongeza kuwa uwepo wa sheria hiyo utaimarisha imani ya taasisi za fedha katika utoaji wa mikopo kwa kutumia mali zinazohamishika, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
“Kupitia mfumo huu mpya, wafanyabiashara wadogo, wakulima na wajasiriamali watapata nafasi ya kupata mikopo bila vikwazo vya dhamana za mali zisizohamishika,” amesisitiza.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchumi wanaamini kuwa muswada huo ukipitishwa na kutekelezwa ipasavyo utaongeza uwekezaji, kukuza biashara ndogo na za kati, pamoja na kuimarisha mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi. Wamesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya mali zinazohamishika kama dhamana ili kuhakikisha fursa hiyo inawanufaisha wananchi wengi zaidi.
