Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

OCPD YATAFSIRI SHERIA 446 KWA KISWAHILI, YAANDAA MISWADA MINNE NA KUCHAPISHA SHERIA NDOGO 447

Imewekwa: 24 April, 2026
OCPD YATAFSIRI SHERIA 446 KWA KISWAHILI, YAANDAA MISWADA MINNE NA KUCHAPISHA SHERIA NDOGO 447

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imeendelea kuimarisha upatikanaji wa haki na uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kukamilisha tafsiri ya sheria kuu 433 kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili, hatua iliyofikisha jumla ya sheria kuu 446 zinazopatikana kwa lugha ya Kiswahili hadi Machi 2026, na kutangazwa rasmi kupitia Tangazo la Serikali Na. 659 la mwaka 2025 na sasa zinatumika katika kuwezesha utoaji wa haki kwa lugha ya Kiswahili pamoja na kuwasaidia wananchi kuelewa sheria za nchi kwa urahisi zaidi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Aprili 24, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

“Katika kuwezesha utekelezaji wa sheria kuu zilizotafsiriwa kwa lugha ya kiswahili, Wizara kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria inaendelea na zoezi la kutafsiri sheria ndogo ambazo katika kipindi cha July 2025 hadi Machi 2026 jumla ya sheria ndogo 229 zimetafsiriwa kutoka lugha ya kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.” Amesema Mh. Dkt. Homera

“Wizara kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imeendelea na majukumu yake katika kuandaa Miswada ya sheria, kusimamia uchapishaji wa sheria ndogo, kutafsiri na kurekebisha sheria. Katika kipindi cha July 2025 hadi machi 2026 wizara kupitia ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imeandaa miswada ya sheria minne kati ya miswada hiyo miwili imesomwa kwa mara ya kwanza ambayo ni mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2026 na mswada wa sheria ya mikopo kwa dhamana za mali zinazohamishika kwa mwaka 2026.” Ameongeza Mh. Dkt. Homera.

Vilevile, amesema OCPD imeandaa, kuhakiki na kuchapisha jumla ya sheria ndogo 447, zikiwemo kanuni 107, notisi 145, amri 125, sheria ndogo 62, hati saba na muongozo mmoja. Sambamba na hilo, ofisi hiyo imekamilisha Toleo la Urekebu la Nyongeza la Mwaka 2025, lililojumuisha sheria kuu 71 zilizorekebishwa pamoja na sheria ndogo 265 zilizofanyiwa urekebu, hatua inayolenga kuimarisha ubora, usahihi na upatikanaji wa sheria nchini.

Kwa mafanikio hayo, OCPD imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza upatikanaji wa haki na kuhakikisha wananchi wanapata sheria zilizo sahihi, zilizo wazi na zinazoeleweka kwa lugha wanayoitumia kila siku. Hatua hizi pia zimeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya wakati na unaochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini