𝗢𝗖𝗣𝗗 𝗬𝗔𝗨𝗡𝗚𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗙𝗔𝗡𝗬𝗔𝗞𝗔𝗭𝗜 𝗞𝗨𝗔𝗗𝗛𝗜𝗠𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗘𝗜 𝗠𝗢𝗦𝗜, 𝗥𝗔𝗜𝗦 𝗦𝗔𝗠𝗜𝗔 𝗔𝗛𝗜𝗠𝗜𝗭𝗔 𝗠𝗦𝗛𝗜𝗞𝗔𝗠𝗔𝗡𝗢 𝗡𝗔 𝗞𝗔𝗭𝗜 𝗭𝗘𝗡𝗬𝗘 𝗦𝗧𝗔𝗛𝗔
Watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wameungana na wafanyakazi wengine nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), katika maadhimisho ya kitaifa yenye kaulimbiu ya "Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050" yaliyofanyika mkoani Njombe na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa mgeni rasmi,
Ushiriki wa OCPD katika maadhimisho hayo umeakisi dhamira ya taasisi ya kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa weledi, uadilifu na uzalendo, sambamba na kuthamini mchango wa watumishi wake katika kuimarisha utawala wa sheria na maendeleo ya Taifa
Akihutubia maelfu ya wafanyakazi na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Rais Samia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha mshikamano, amani na utulivu ili kulinda mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana nchini, akisisitiza kuwa kazi ni zaidi ya kipato, bali ni msingi wa heshima, utu na ustawi wa Taifa
"Kazi haiwezi kuwa na staha bila amani na hakuna ustawi wa wafanyakazi bila utulivu, Taifa letu linahitaji mshikamano, tufanye kazi kwa pamoja, tujenge heshima ya nchi yetu na kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha wote," alisema Rais Samia
Aidha, Rais Samia alieleza kuwa ajira zenye staha zinapaswa kuzingatia heshima, usalama, kipato cha haki na mazingira bora yanayolinda utu wa mfanyakazi, akibainisha kuwa kazi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwataka wafanyakazi nchini kuendelea kuwa wavumilivu, kujituma na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku
"Niwasihi wafanyakazi kutokata tamaa, wananchi wanawategemea, hivyo ni muhimu kuendelea kutoa huduma kwa bidii, uvumilivu na kujitolea hata pale changamoto zinapojitokeza," alisisitiza Waziri Mkuu
Ushiriki wa OCPD katika maadhimisho haya unaendelea kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi wake na kuakisi dhamira ya Ofisi ya kuendelea kutoa huduma bora za kisheria kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla, hatua inayochochea ujenzi wa jamii inayozingatia haki, usawa na maendeleo endelevu
Maadhimisho ya Mei Mosi yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa wafanyakazi katika ujenzi wa Taifa, kuhimiza uwajibikaji, ubunifu na kujituma, na kuendeleza ari ya pamoja katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ustawi wa Watanzania wote
