Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗪𝗔𝗝𝗨𝗠𝗕𝗘 𝗪𝗔 𝗠𝗘𝗡𝗘𝗝𝗜𝗠𝗘𝗡𝗧𝗜 𝗬𝗔 𝗢𝗙𝗜𝗦𝗜 𝗬𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗠𝗞𝗨𝗨 𝗪𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 𝗪𝗔𝗣𝗘𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗙𝗨𝗡𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗠𝗔𝗦𝗨𝗔𝗟𝗔 𝗬𝗔 𝗨𝗞𝗔𝗚𝗨𝗭𝗜 𝗡𝗔 𝗡𝗔𝗠𝗡𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗨𝗗𝗛𝗜𝗕𝗜𝗧𝗜 𝗩𝗜𝗛𝗔𝗧𝗔𝗥𝗜𝗦𝗛𝗜

Imewekwa: 02 May, 2026
𝗪𝗔𝗝𝗨𝗠𝗕𝗘 𝗪𝗔 𝗠𝗘𝗡𝗘𝗝𝗜𝗠𝗘𝗡𝗧𝗜 𝗬𝗔 𝗢𝗙𝗜𝗦𝗜 𝗬𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗠𝗞𝗨𝗨 𝗪𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 𝗪𝗔𝗣𝗘𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗙𝗨𝗡𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗠𝗔𝗦𝗨𝗔𝗟𝗔 𝗬𝗔 𝗨𝗞𝗔𝗚𝗨𝗭𝗜 𝗡𝗔 𝗡𝗔𝗠𝗡𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗨𝗗𝗛𝗜𝗕𝗜𝗧𝗜 𝗩𝗜𝗛𝗔𝗧𝗔𝗥𝗜𝗦𝗛𝗜

Menejimenti ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imepata mafunzo maalum ya masuala ya ukaguzi na namna ya kutambua, kuchambua, kutathmini na kudhibiti vihatarishi katika eneo la kazi.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Kaimu Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bi. Rehema Katuga mkoani Morogoro.

Akifungua mafunzo hayo Bi. Rehema amesema kuwa ukaguzi wa ndani ni jicho la taasisi katika kuangalia majukumu yanatekelezwa kwa mujibu wa kanuni za nchi.

"Ukaguzi wa ndani ni jicho ambalo linaangalia kama taasisi inatekeleza majukumu yake kwa kanuni za nchi ili kupata matokeo mazuri," amesema Bi. Rehema.

Kaimu Mwandishi Mkuu wa Sheria, ameendelea kwa kuitaka menejimenti na watumishi kuwapa ushirikiano kitengo cha ukaguzi wa ndani na kamati ya ukaguzi wa ndani.

"Tutoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati na kitengo cha ukaguzi kwani wanahakikisha OCPD inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, tunaamini mtatusaidia sana kwa yale ambayo hatujayaona, kuweni huru kutushauri na sisi tutayapokea," ameeleza Kaimu Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Bi. Katuga ameendelea kwa kusema kuwa Serikali inategemea sana Ofisi katika kuandika Sheria fasaha na zinazotekelezeka.

"Kama ofisi tunategemewa sana na serikali kwani hakuna jambo linalofanyika nchini bila sheria hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha imani tunayopewa na serikali inatimia kwa kutoa sheria fasaha," ameongeza Bi. Rehema.

Mafunzo haya ni ya siku mbili ambayo yataambatana na uzinduzi wa kamati ya ukaguzi ya OCPD.