Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗦𝗛𝗜𝗡𝗬𝗔𝗡𝗚𝗔 𝗬𝗔𝗡𝗨𝗙𝗔𝗜𝗞𝗔 𝗡𝗔 𝗘𝗟𝗜𝗠𝗨 𝗬𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 𝗞𝗨𝗣𝗜𝗧𝗜𝗔 𝗢𝗖𝗣𝗗

Imewekwa: 14 May, 2026
𝗦𝗛𝗜𝗡𝗬𝗔𝗡𝗚𝗔 𝗬𝗔𝗡𝗨𝗙𝗔𝗜𝗞𝗔 𝗡𝗔 𝗘𝗟𝗜𝗠𝗨 𝗬𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 𝗞𝗨𝗣𝗜𝗧𝗜𝗔 𝗢𝗖𝗣𝗗

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imeendelea kushiriki katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Shinyanga na kufanya ziara ya kikazi iliyolenga kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na kutoa elimu kuhusu majukumu ya Ofisi katika sekta ya sheria, ziara iliyofanyika Mei 13, 2026 chini ya uongozi wa Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Tafiti na Mafunzo, Bi. Nyambuli Tungaraja, akiwa ameambatana na Mawakili wa Serikali pamoja na Waandishi wa Sheria.

Katika ziara hiyo OCPD imekutana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambapo pamoja na kuwasilisha salamu za Ofisi hiyo, walitoa ufafanuzi kuhusu majukumu makuu ya OCPD ikiwemo uandishi wa sheria, utafsiri wa sheria na urekebu wa sheria kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanazielewa sheria za nchi pamoja na mifumo ya utekelezaji wake, ambapo pia OCPD imeeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na viongozi wa mikoa katika kuwafikia wananchi kupitia huduma za elimu ya sheria.

Akizungumza katika kikao hicho, Nyambuli Tungaraja amesema kuwa wakuu wa mikoa ni wadau muhimu katika utekelezaji wa masuala ya sheria na utawala bora, hivyo OCPD itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katika kuwafikishia wananchi elimu na huduma za kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Sambamba na ziara hiyo, OCPD imepata pia fursa ya kubadilishana uzoefu na Meneja wa Mkoa wa PSSSF Shinyanga kuhusu namna taasisi mbalimbali zinavyoweza kushirikiana katika kuwahudumia wananchi na kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na kijamii ambapo kupitia kampeni hiyo Serikali inaendelea kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ili kuimarisha upatikanaji wa haki nchini.