π πππ¨ππ¨π π¨ π¬π π’ππ£π π‘π π§π¨π π π¬π ππ¨π₯ππππππ¦ππ π¦πππ₯ππ π¬ππππππ‘π¨πππͺπ
Mawakili wa Serikali wanaoshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Arusha, wamepata ufafanuzi kuhusu tofauti ya majukumu kati ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mafunzo yanayoendelea jijini humo.
Ufafanuzi huo umetolewa leo Mei 20, 2026 na Mwandishi Mkuu wa Sheria wa, Bw. Onorius Njole, wakati akitoa mada kuhusu “Uandishi wa Sheria na Uendeshaji wa Mashauri katika Utendaji wa Kisasa wa Umma”, ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa Mawakili kuanzia Mei 18 hadi 20, 2026.
Akijibu swali lililotaka kufahamu tofauti ya majukumu ya taasisi hizo mbili, Bw. Njole amesema Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria inajihusisha zaidi na uandishi wa sheria kwa kuzingatia maelekezo yanayotoka katika wizara, taasisi za Serikali ikiwa ni pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria, huku Tume hiyo ikiwa na jukumu la kufanya tafiti kuhusu sheria zilizopo ili kubaini changamoto na uhitaji wa maboresho kulingana na mabadiliko ya jamii na wakati.
Amesema matokeo ya tafiti zinazofanywa na Tume ya Kurekebisha Sheria huwasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kabla ya kupelekwa katika wizara husika kwa ajili ya utekelezaji, kwa kuwa kila sheria ina wizara inayohusika moja kwa moja na umiliki wa utekelezaji wake.
“Sisi OCPD tunafanya kazi kwa kuzingatia maelekezo yanayotoka katika maeneo mbalimbali ikiwemo Tume ya Kurekebisha Sheria. Hata hivyo, tafiti zote zinazofanywa lazima zipitie katika wizara husika kwa sababu kila sheria ina mmiliki wake,” alisema Bw. Njole.
Katika mada yake, Bw. Njole pia aliwaelekeza washiriki kuhusu historia ya Ofisi na majukumu yake makuu ambayo ni Uandishi wa Sheria, Ufasili wa Sheria pamoja na Urekebu wa Sheria, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya uandishi wa sheria unaoeleweka kwa wananchi na unaokwenda sambamba na mahitaji ya utendaji wa kisasa wa umma, ikiwemo matumizi ya lugha sahihi, uwazi wa vifungu vya sheria na kuzingatia mazingira halisi ya utekelezaji wa sheria hizo.
Baada ya mada hiyo, baadhi ya washiriki waliomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa mara kwa mara kutokana na umuhimu wake katika kuongeza uelewa na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma. Akijibu ombi hilo, Bw. Njole alisema mafunzo hayo hutolewa kila Jumatatu katika Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, huku akieleza kuwa atawasiliana na Menejimenti kuona namna ya kuwashirikisha pia wadau kutoka nje ya Ofisi kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo.
