Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA YAKABIDHI JUZUU ZA TOLEO LA UREKEBU LA MWAKA 2023

Imewekwa: 13 September, 2025
OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA YAKABIDHI JUZUU ZA TOLEO LA UREKEBU LA MWAKA 2023

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imekabidhi Juzuu za Toleo la Urekebu wa Sheria la mwaka 2023 kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kupongeza mchango mkubwa uliotolewa na Ofisi hiyo kupitia watumishi wake kwenye utekelezaji wa zoezi la Urekebu.

Akikabidhi Juzuu hizo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu,Tafiti na Mafunzo kwa naiaba ya  Mwandishi Mkuu wa Sheria Bi. Rehema Katuga amepongeza ushirikiano mkubwa ambao Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeutoa wakati wa mchakato mzima wa utekelezaji wa zoezi hilo na kuchangia kukamilika kwa zoezi hilo la kihistoria.

“Wakati tunaanza zoezi hili Ofisi yetu ilikuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa watumishi hasa Mawakili wa kufanya kazi hii lakini tulikuwa tukibisha hodi kwenye Ofisi yako kuomba Mawakili kuja kushirikiana nasi katika kutekeleza zoezi hili, na hakika walitusaidia sana hadi tumekamilisha” alieleza Bi. Katuga.

Aliongeza“ Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kutambua mchango wenu imeona ni muhimu na Ofisi yako pia ipate nakala hizi ingawa tunatambua kuwa tumeleta chache kutokana na gharama lakini ziwasaidie kwa kuanzia na kuwa kama kumbukumbu kwenu, lakini mnaweza kupata nakala laini zote kupitia mfumo wa OAGMIS” Alieleza Bi. Katuga.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Divisheni ya Urekebu,Tafiti na Mafunzo ameongeza kuwa pamoja na nakala hizo tano pia wameipatia Ofisi hiyo tuzo maalumu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kutambua mchango wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika zoezi hilo la Urekebu wa Sheria.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi yake Mkurugenzi wa Mashtaka Bwana Sylvester Mwakitalu amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) na kushukuru  kwa kuwapatia nakala hizo za kuanzia kwa ajili ya Ofisi yake maana wangeenda kununua dukani ingekuwa gharama kubwa.

“Ofisi yetu tunatumia Sheria hizi kila siku maana tunatoa huduma za mashtaka kwenye mahakama zote nchini hasa hasa mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi ndiko tunaenda kila siku, lakini pia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, kwahiyo hizi Sheria ni nyenzo muhimu sana kwetu” Alieleza Bwana Mwakitalu.

Aliongeza” Nakala hizi tulizozipata tutazisambaza kwa Mawakili wetu kwanza, alafu sisi tutaendela kusubiria kupata zingine kwa utaratibu maalumu lakini pia kwa kutumia zile ambazo zinazopatikana kwenye mfumo wa nakala tete”.

Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023 lilizinduliwa kwa mujibu wa Sheria na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi wanne mwaka huu na kutangaza kuanza kutumika tarehe 1 Julai 2025 na hivyo kufuta Toleo la sheria la mwaka mwaka 2002.