Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗦𝗘𝗥𝗜𝗞𝗔𝗟𝗜 𝗬𝗔𝗭𝗜𝗗𝗜 𝗞𝗨𝗜𝗠𝗔𝗥𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗨𝗣𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔𝗡𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗛𝗔𝗞𝗜 𝗞𝗨𝗣𝗜𝗧𝗜𝗔 𝗞𝗔𝗠𝗣𝗘𝗡𝗜 𝗠𝗦𝗔𝗜𝗗𝗔 𝗪𝗔 𝗛𝗨𝗗𝗨𝗠𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 - 𝗔𝗪𝗔𝗠𝗨 𝗬𝗔 𝗣𝗜𝗟𝗜

Imewekwa: 21 June, 2026
𝗦𝗘𝗥𝗜𝗞𝗔𝗟𝗜 𝗬𝗔𝗭𝗜𝗗𝗜 𝗞𝗨𝗜𝗠𝗔𝗥𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗨𝗣𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔𝗡𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗛𝗔𝗞𝗜 𝗞𝗨𝗣𝗜𝗧𝗜𝗔 𝗞𝗔𝗠𝗣𝗘𝗡𝗜 𝗠𝗦𝗔𝗜𝗗𝗔 𝗪𝗔 𝗛𝗨𝗗𝗨𝗠𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 - 𝗔𝗪𝗔𝗠𝗨 𝗬𝗔 𝗣𝗜𝗟𝗜

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili ambayo imezinduliwa tarehe 20 Juni 2026 katika Uwanja wa Dole, Kizimbani Zanzibar, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mh. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uzinduzi huo rasmi.

Katika hafla hiyo, Mh. Dkt. Mwinyi alitembelea banda la OCPD na kupata maelezo kuhusu huduma mbalimbali za kisheria zinazotolewa na ofisi hiyo kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu na usaidizi wa kisheria kwa urahisi na kwa wakati.

Katika uzinduzi huo, Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali, Bw. Onorius Njole, alishiriki pamoja na viongozi wengine wa Serikali na taasisi mbalimbali za sekta ya sheria ikiwa ni pamoja na kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ili kujionea huduma zinazotolewa kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mh. Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wengi zaidi nchini.

"Serikali imechukua hatua za makusudi za kuimarisha huduma za msaada wa kisheria, kwa kutunga sera itakayotoa mwongozo wa usimamizi na uendeshaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini, hatua itakayoleta mabadiliko makubwa ya kimtazamo na kimfumo katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria," amesema Mh. Dkt. Mwinyi.

Ameongeza kuwa hatua hiyo itawezesha wananchi kupata huduma za kisheria kwa urahisi zaidi huku ikichangia kuimarisha upatikanaji wa haki, kuimarisha utawala bora na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mh. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.

"Wizara kwa kushirikiana na taasisi zingine katika utekelezaji wa kampeni, itahakikisha huduma zinasogezwa karibu katika maeneo mbalimbali nchini," amesema Mh. Dkt. Homera.

Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa kuwafikishia huduma za kisheria moja kwa moja katika maeneo wanayoishi na kufanyia shughuli zao za kila siku.

 

Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia umezikutanisha taasisi mbalimbali za sekta ya sheria kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zikiwa na lengo la kutoa elimu ya sheria, ushauri wa kisheria na huduma nyingine zinazochangia kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Kupitia ushiriki wake katika kampeni hiyo, OCPD imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya sheria pamoja na ushauri wa kisheria unaowasaidia wananchi kuelewa na kulinda haki zao kwa mujibu wa sheria.