Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗢𝗖𝗣𝗗 𝗬𝗔𝗨𝗡𝗚𝗔 𝗠𝗞𝗢𝗡𝗢 𝗞𝗔𝗠𝗣𝗘𝗡𝗜 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝟮𝟳 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗝𝗔𝗡𝗜, 𝗬𝗔𝗭𝗜𝗡𝗗𝗨𝗔 𝗦𝗛𝗜𝗡𝗗𝗔𝗡𝗢 𝗟𝗔 #𝗠𝗧𝗜𝗪𝗔𝗡𝗚𝗨 𝗖𝗛𝗔𝗟𝗟𝗘𝗡𝗚𝗘

Imewekwa: 27 June, 2026
𝗢𝗖𝗣𝗗 𝗬𝗔𝗨𝗡𝗚𝗔 𝗠𝗞𝗢𝗡𝗢 𝗞𝗔𝗠𝗣𝗘𝗡𝗜 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝟮𝟳 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗝𝗔𝗡𝗜, 𝗬𝗔𝗭𝗜𝗡𝗗𝗨𝗔 𝗦𝗛𝗜𝗡𝗗𝗔𝗡𝗢 𝗟𝗔 #𝗠𝗧𝗜𝗪𝗔𝗡𝗚𝗨 𝗖𝗛𝗔𝗟𝗟𝗘𝗡𝗚𝗘

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ikiongozwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo, Bi. Rehema Katuga aliyemwakilisha Mwandishi Mkuu wa Sheria, leo tarehe 27.06.2026 imeshiriki zoezi la upandaji miti katika Kituo cha Afya cha Ilazo jijini Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kuhifadhi mazingira kupitia Kampeni ya  27 ya Kijani inayoratibiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza na TBC wakati wa zoezi hilo, Bi. Katuga amesema OCPD inajivunia kuwa sehemu ya kampeni hiyo kwa kuwa inalenga kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuimarisha utunzaji wa mazingira, huku akisisitiza kuwa ofisi itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

"Sisi OCPD tunafurahi kuwa sehemu ya kampeni hii ambayo itasaidia kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuimarisha mazingira" amesema Bi. Katuga.

Katika kuendeleza dhamira hiyo, Bi. Katuga ameitambulisha rasmi #MtiWangu Challenge, mpango unaowahamasisha watumishi wa OCPD kupanda miti majumbani kwao na kuhakikisha inakua,

"Tunataka pia kuhamasisha watumishi wa OCPD katika kuifanya Dodoma ya kijani, hivyo kupitia hii challenge ya #MtiWangu watumishi wanapewa miti kwenda kuipanda majumbani na tutafanya ufuatiliaji ambapo mwakani watumishi ambao miti yao itakuwa imekua vizuri watapatiwa zawadi nono". Alisisitiza Bi. Katuga

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ilazo, Mathei Kauki, ameishukuru OCPD kwa kuchagua kituo hicho kwa ajili ya zoezi la upandaji miti, akieleza kuwa miti hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa.

"Miti ya matunda na miti ya vivuli iliyopandwa na OCPD kituoni hapa ina msaada mkubwa kwa wagonjwa ambapo itawawezesha kupata vivuli, matunda na upepo na inakuwa ni faraja kwao” amesema Kauki.

Kupitia ushiriki wake katika Kampeni ya Tanzania 27 ya Kijani pamoja na uzinduzi wa #MtiWangu Challenge, OCPD inalenga kuhamasisha utamaduni wa upandaji na utunzaji wa miti miongoni mwa watumishi wake na jamii kwa ujumla ili kuongeza mchango katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa pamoja, OCPD na uongozi wa Kituo cha Afya cha Ilazo wameahidi kuisimamia na kuitunza miti yote iliyopandwa ili ikue na kustawi vizuri kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.