Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

π—₯π—”π—œπ—¦ π—ͺ𝗔 𝗝𝗔𝗠𝗛𝗨π—₯π—œ 𝗬𝗔 π— π—¨π—¨π—‘π—šπ—”π—‘π—’ π—ͺ𝗔 π—§π—”π—‘π—­π—”π—‘π—œπ—” π—”π—”π—šπ—œπ—­π—” π—¦π—›π—˜π—₯π—œπ—” π—­π—œπ—Ÿπ—œπ—­π—’π—§π—”π—™π—¦π—œπ—₯π—œπ—ͺ𝗔 π—žπ—ͺ𝗔 π—Ÿπ—¨π—šπ—›π—” 𝗬𝗔 π—žπ—œπ—¦π—ͺπ—”π—›π—œπ—Ÿπ—œ π—žπ—¨π—™π—œπ—žπ—œπ—” π—ͺπ—”π—‘π—”π—‘π—–π—›π—œ

Imewekwa: 15 July, 2026
π—₯π—”π—œπ—¦ π—ͺ𝗔 𝗝𝗔𝗠𝗛𝗨π—₯π—œ 𝗬𝗔 π— π—¨π—¨π—‘π—šπ—”π—‘π—’ π—ͺ𝗔 π—§π—”π—‘π—­π—”π—‘π—œπ—” π—”π—”π—šπ—œπ—­π—” π—¦π—›π—˜π—₯π—œπ—” π—­π—œπ—Ÿπ—œπ—­π—’π—§π—”π—™π—¦π—œπ—₯π—œπ—ͺ𝗔 π—žπ—ͺ𝗔 π—Ÿπ—¨π—šπ—›π—” 𝗬𝗔 π—žπ—œπ—¦π—ͺπ—”π—›π—œπ—Ÿπ—œ π—žπ—¨π—™π—œπ—žπ—œπ—” π—ͺπ—”π—‘π—”π—‘π—–π—›π—œ

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amepongeza na kutambua jitihada za kuendeleza huduma za kisheria ikiwemo kazi ya kutafsiri sheria katika lugha ya kiswahili kwani hatua hii itasaidia mwananchi kuielewa sheria na haki zake.

Mhe. Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha mawakili wa serikali kilichofanyika tarehe 13, Julai 2026, jijini Arusha.

"Natambua jitihada zenu za kuendeleza huduma za msaada wa kisheria ikiwemo kazi ya kutafsiri sheria katika lugha ya kiswahili na nimeambiwa kazi inakaribia kumalizika na sasa wameniomba kuja kuzindua sheria hizi kwa lugha ya kiswahili na mimi nasema nipo tayari kufanya hivyo," amesema Mhe. Rais Samia

Rais Samia ameendelea kwa kusema kuwa zoezi la tafsiri ya sheria itamsaidia mwananchi kuelewa haki zake, sheria na mipaka yake.

"Hatua hii mliyochukua ni muhimu na ya kupongezwa kwani mwananchi anapo ielewa sheria anaelewa haki zake, wajibu wake, mipaka ya uhuru wake na mipaka ya mamlaka ya serikali na hii ndio maana halisi ya utawala wa sheria," ameongeza Mhe. Rais Samia

Mhe. Rais Samia ameelekeza zoezi hili lisiishie kwenye kutafsiri sheria tu bali kuhakikisha kufuata watu na kuhakikisha wanaelewa sheria hizo.

"Kazi yenu isiishie tu kuzitafsiri lakini pia muingie njiani kwenda kuzifundisha kwa watu, watu wazielewe, wazifahamu na wajue mipaka ya serikali, mipaka yao na sheria za nchi yao zinasema nini. Kwahiyo ni matumaini yangu kuwa hatua hizi zote mlizozichukua zitakua chachu ya kuongeza ubora, ufanisi, nidhamu na weledi katika kutoa huduma za kisheria ndani ya serikali na kwa wananchi kwa ujumla," ameelekeza Mhe. Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kwa kusema kuwa hatua hizi pamoja na nyingine zinapaswa kuendana na malengo tuliyojiwekea katika dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 ambayo tumeanza utekelezaji wake mwaka huu.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Bw. Bavoo Junus amesema kuwa jumla ya sheria kuu 433 zimetafsiriwa kwa lugha ya kiswahili na zimetangazwa rasmi kupitia gazeti la serikali namba 659 la mwaka 2025. 

"Kukamilika kwa zoezi hili la tafsiri kutaongeza wigo wa upatikanaji wa haki, utaongeza uwezo wa serikali kusimamia na kutekeleza sheria zake kwa ufanisi zaidi, kutaimarisha utawala wa sheria na kuongeza ufanisi wa taasisi za umma na kutekeleza kwa vitendo malengo ya dira ya taifa ya maendeleo 2050," amesema Bw. Bavoo