Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

𝗒𝗖𝗣𝗗 𝗑𝗔 π——π—Ÿπ—¦ π—ͺ𝗔π—ͺπ—˜π—žπ—” π— π—œπ—žπ—”π—žπ—”π—§π—œ 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—•π—’π—₯π—˜π—¦π—›π—” π— π—–π—›π—”π—žπ—”π—§π—’ π—ͺ𝗔 π—¨π—”π—‘π——π—œπ—¦π—›π—œ π—ͺ𝗔 π—¦π—›π—˜π—₯π—œπ—” π—‘π—–π—›π—œπ—‘π—œ

Imewekwa: 12 October, 2026
𝗒𝗖𝗣𝗗 𝗑𝗔 π——π—Ÿπ—¦ π—ͺ𝗔π—ͺπ—˜π—žπ—” π— π—œπ—žπ—”π—žπ—”π—§π—œ 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—•π—’π—₯π—˜π—¦π—›π—” π— π—–π—›π—”π—žπ—”π—§π—’ π—ͺ𝗔 π—¨π—”π—‘π——π—œπ—¦π—›π—œ π—ͺ𝗔 π—¦π—›π—˜π—₯π—œπ—” π—‘π—–π—›π—œπ—‘π—œ

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imekutana na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Sheria (DLS) kutoka Wizara mbalimbali na baadhi ya taasisi za Serikali, kujadili mikakati ya kuboresha mchakato wa uandishi wa sheria nchini, ikiwemo kuimarisha ushirikiano, kuongeza ufanisi katika maandalizi ya mapendekezo ya sheria na kuhakikisha sheria zinaendana na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

Akifungua kikao hicho, Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD), Bw. Onorius Njole, amesema kikao hicho ni muhimu katika kutathmini mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa uandishi wa sheria, pamoja na kujadiliana hatua za kuboresha utekelezaji wa majukumu yanayohusiana na mchakato huo.

“Kwenye kikao hiki muhimu tunaenda kujadiliana mambo mbalimbali, mafanikio na changamoto katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa uandishi wa sheria, kikao chetu ni muhimu na tunayo mengi ya kujadiliana na kuona ni namna gani tunaweza kuboresha utekelezaji wa majukumu ya uandishi wa sheria,” amesema Bw. Njole.

Amesisitiza kuwa uandishi wa sheria ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya OCPD, wanasheria wa Wizara na taasisi za Serikali katika hatua mbalimbali za maandalizi, utungaji na marekebisho ya sheria, ili kuhakikisha mchakato huo unatekelezwa kwa ufanisi na kutoa sheria zilizoandaliwa kwa ubora unaotakiwa.

“Jukumu la uandishi wa sheria ni letu sote, nategemea katika kikao hiki tutakuwa na mijadala itakayopelekea ushirikiano baina yetu na mwisho tuwe na mfumo ambao umejengwa kwa sheria fasaha na utekelezaji bora ili kufikia malengo,” ameongeza Bw. Njole.

Akizungumzia umuhimu wa uandishi wa sheria katika maendeleo ya Taifa, Bw. Njole amesema kuwa mchakato huo una nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuhakikisha sheria zinazoandaliwa au kufanyiwa marekebisho zinaendana na malengo ya maendeleo yaliyowekwa.

“Mchakato wa uandishi wa sheria ni muhimu katika utekelezaji wa Dira 2050 kwani kuna baadhi ya sheria zinatakiwa kuandikwa upya au kufanyiwa marekebisho ili kurahisisha utekelezaji wa Dira kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ameeleza Bw. Njole.

Aidha, amebainisha kuwa sheria zina mchango muhimu katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Sheria kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mahitaji ya kisera na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria, Bi. Chresencia Mathayo, amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Sheria kuhakikisha sheria zinazosimamiwa katika Wizara na taasisi zao zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku wakitoa ushauri wa kitaalamu pale wanapobaini sheria zinazohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuendana na mwelekeo huo wa maendeleo.

“Tuhakikishe sheria tunazosimamia kwenye Wizara zetu zinaendana na Dira ya Taifa na kama kuna sheria ambayo haiendani na utekelezaji wa Dira basi tuwe wepesi kushauri kuhusu sheria hiyo,” amesema Bi. Mathayo.

Katika kuimarisha ufanisi wa mchakato wa uandishi wa sheria, kikao hicho kimeazimia kuimarisha ushirikiano kati ya OCPD na Idara na Vitengo vya Sheria vya Wizara na taasisi za Serikali katika hatua zote za utungaji na marekebisho ya sheria, huku Wakuu wa Idara na Vitengo vya Sheria wakitakiwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha maafisa walio chini yao wanauelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uandishi wa sheria.