KONGAMANO LA NNE LA KITAIFA LA WIKI YA UFUATILIAJI, TATHMINI NA KUJIFUNZA (MEL)

Watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) washiriki Kongamano la Nne la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) lililofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa jijini Mwanza.
Akifungua kongamano hilo, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alisisitiza kuanzishwa kwa Vitengo vya Tathimni na Ufuatiliaji kwenye Wizara zote, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote kwani Kitengo hicho ni kiungo muhimu katika kuchochea utekelezaji wa majukumu ya Serikali unaombatana na matokeo zaidi kuliko mchakato.
“Vitengo hivi ni kiungo muhimu katika kuchochea utekelezaji wa majukumu ya serikali vinavyolenga matokeo badala ya mchakato lakini pia vinasaidia kupima ufanisi wa Taasisi katika utekelezaji wa shabaha zake, kupima na kuchochea mienendo ya watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao na kujenga uwanda mpana wa jamii katika kushiriki shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi na mwisho wa siku kupitia mifumo hii, tutajenga uwazi, uwajibikaji, na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa tija,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wameeleza namna ushiriki wao unavyowasaidia katika kupanua uelewa na kupata mbinu mpya za kiutendaji kwenye Ofisi zao kwa kubadilishana mawazo na watumishi kutoka kwenye Taasisi zingine zilizoshiriki pamoja na kutoa uzoefu wa namna njema ya kuteleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza tija kwenye Taasisi.
“Kongamano hili limetupa nafasi ya kujifunza mbinu bunifu za MEL ambazo tunaweza kuzitumia katika kutoa ushauri wa kisheria na kuhakikisha sera na sheria zinazopitishwa zinaendana na mifumo ya uwajibikaji na tathmini ya kitaifa,” alisema Bi. Frida Peter Mwera.