OCPD YAANZA UREKEBU WA SHERIA NDOGO

Waandishi wa sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (OCPD) wameanza zoezi la utambuzi wa sheria ndogo zote zilizotungwa kuanzia mwaka 1961 hadi 2025 ikiwa ni mwanzo wa zoezi kubwa la Urekebu wa sheria ndogo zote nchini.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa divisheni ya Urekebu Utafiti na mafunzo Mick Modestus Chotta amesema zoezi hilo ni hatua ya mwanzo kuelekea zoezi kubwa la Urekebu wa sheria ndogo, ambapo wanazichambua na kuzitambua sheria ndogo zote zilizotungwa toka mwaka 1961 hadi sasa.
“Tangu mwaka 1961, zipo sheria ndogo zilizotungwa chini ya sheria mama ambazo baadaye zilifutwa. Sheria hizo tutazitambua lakini hazitajumuishwa katika zoezi la urekebu. Vilevile, zipo sheria ndogo zilizotungwa tangu miaka hiyo ambazo bado zipo hai hadi leo; hizi ndizo tutakazozijumuisha kwenye zoezi la urekebu,” alisema Bw. Chotta.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la utambuzi, OCPD itakuwa na orodha kamili ya sheria ndogo zote zinazotumika ambazo zitaingizwa kwenye zoezi kubwa la urekebu. Katika hatua hiyo, kila sheria itapitiwa kwa kina na kujumuisha marekebisho yote yaliyowahi kufanyika tangu kutungwa kwake, na hivyo kupata Toleo la Urekebu wa Sheria Ndogo za Mwaka 2025.
Zoezi hili linafanyika kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na wataalamu wengine kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, likiwa na lengo la kuhakikisha kuwa mchakato wa urekebu unatekelezwa kwa wakati, na kuzingatia ubora wa hali ya juu, kwa kuimarisha urahisi wa upatikanaji na matumizi ya sheria ndogo nchini.
Zoez la Utambuzi wa sharia ndogo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kuhakikisha kuwa mfumo wa sheria nchini unakuwa wa kisasa, unaoeleweka, na unaendana na mazingira ya sasa.