Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD YAANZA MCHAKATO WA KUTENGENEZA MFUMO WA UANDISHI WA SHERIA NCHINI.

Imewekwa: 19 October, 2025
OCPD YAANZA MCHAKATO WA KUTENGENEZA MFUMO WA UANDISHI WA SHERIA NCHINI.

Waandishi wa sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wakutana kuandaa mahitaji muhimu kama hatua ya awali ya utengenezaji wa Mfumo wa Uandishi wa Sheria nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Divisheni ya Uandishi wa Sheria, Bw. Shaban Kabunga wakati akizungumza kwenye mkutano huo muhimu unaoendelea Jijini Arusha.

“Mfumo wa Uandishi wa Sheria tunaoutaka nchini kwetu hauwezi  kuanza  kuutengeneza bali kwanza tunahitaji kubaini mahitaji yetu muhimu tunayotaka yaingizwe kwenye mfumo huo kutoka katika idara zote kuu tatu yaani Idara ya Uandishi wa Sheria, Idara ya Urekebu wa Sheria na Idara ya Ufasili ya Sheria. Mahitaji hayo ndiyo yatapelekea kuwa na mfumo jumuishi wenye moduli za uandishi, ufasili na urekebu wa sheria. Moduli hizo zitabainisha namna mfumo huo utakavyofanya kazi hatua kwa hatua” amesema Kabunga.

Ameongeza “Baada ya kila idara kuwa na mahitaji, hatua inayofuata tutakaa pamoja idara zote kwa uwakilishi na kujumuisha mahitaji yetu kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kuzingatia matakwa yao ili mwisho wa siku tuweze kupata mfumo thabiti unaoakisi mchakato mzima wa uandishi wa sheria, urekebu na ufasiri wa sheria unaotekelezwa na Ofisi ya Uandishi wa Sheria”.

Aidha Kabunga amebainisha kuwa hatua hiyo ya sasa ni muhimu na inalenga kuonesha njia kwa Idara zingine namna zoezi hilo litakavyofanyika ili kuhakikisha kuwa mahitaji yote yanatambuliwa kabla ya kuanza kuandaa mfumo jumuishi na hivyo kuwezesha nchi kupata mfumo bora na madhubuti kulingana na taratibu na mtindo wa uandishi wa sheria Nchini.

Amesema kila nchi ina mtindo wake wa uandishi wa sheria na kutofautiana mchakato wa uandishi wa sheria. Hivyo, huwezi kuutumia mfumo mzima unaotumika nchi nyingine kuandika sheria, ni lazima kwanza ubainishe mahitaji ya nchi yako yanayo akisi mtindo wa uandishi wa sheria na mchakato wa utungaji wa sheria. Mifumo ya nchi nyingine itasaidia kwa maeneo yanayofana na mahitaji yetu. Kwa utaalamu tulionao nchini, ninaamini tunaweza kuanza kutengeneza mfumo wa uandishi wa sheria, na pale itakapohitajika, tutaona namna ya kupata utaalamu kutoka nje ili kuweka sawa mfumo huo.

Kaimu Mkurugenzi amesema Tanzania itakuwa moja ya nchi chache barani afrika ambazo zina mfumo huo maalumu wa uandishi wa sheria na hivyo kurahisha zoezi la uandishi wa sheria na ufikiwaji wa sheria hizo kwa urahisi.