Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

MAWAKILI WA SERIKALI WASHIRIKI MAFUNZO YALIYOANDALIWA NA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Imewekwa: 21 August, 2024
MAWAKILI WA SERIKALI WASHIRIKI MAFUNZO YALIYOANDALIWA NA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OMMS) iliandaa mafunzo ya siku sita (6) kwa kwa Mawakili wa Serikali. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma kuanzia tarehe 27 Mei, 2024 hadi Juni mosi, 2024. Lengo la mafunzo hayo ni kukuza uwezo wa Mawakili wa Serikali katika utoaji wa huduma bora za kisheria, kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili waweze kuendana na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika sekta mbalimbali ambayo yamesababisha kuwepo kwa mabadiliko ya sheria na kuimarisha weledi wa Mawakili wa Serikali ili kuhakikisha kunakuwa na utawala wa sheria na utawala bora kwa ajili ya ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mwitikio wa kuhudhuria mafunzo kwa Mawakili wa Serikali ulikuwa ni mkubwa kiasi cha kufanya Kamati ya uratibu wa mafunzo kubadilisha sehemu ya kufanyia mafunzo hayo. Hata hivyo, jumla ya awakili wa Serikali 290 washiriki katika mafunzo na kupewa vyeti vya ushiriki.

Mafunzo haya yalifunguliwa tarehe 27 Juni, 2024 na Mgeni Rasmi Mhe. George Boniphace Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Hata hivyo, katika hotuba yake ya ufunguzi alieleza kuwa, sheria ndio nyenzo kuu katika upatikanaji wa haki za watu na Serikali, hivyo nchi yoyote ya kidemokrasia lazima izingatie utawala wa sheria na utawala bora.

Katika mafunzo haya mada takribani kumi na tatu (13) ziliwasilishwa na hoja mbalimbali ziliibuliwa, kujadiliwa na kutolewa ufafanuzi na wataalam wabobevu katika maeneo mbalimbali ya kisheria ikiwemo majadiliano ya mikataba na migogoro ya kitaifa na kimataifa, uandishi wa sheria, utoaji wa ushauri wa kisheria na changamoto za mashauri katika mabaraza na mahakama za kimataifa.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa katika mafunzo hayo kama vile, mbinu zinazotumika kutafsiri sheria, masuala muhimu ya kuzingatia wakati kuishauri serikali, masuala muhimu ya kuzingatia katika majadiliano ya mkataba, wajibu wa Wakili wa Serikali katika kuzuia na kutatua mashauri ya madai dhidi ya Serikali, mwongozo madhubuti kwenye taratibu za ununuzi wa umma kwa Mawakili wa Serikali, misingi ya uandishi wa sheria, uandaaji wa sera madhubuti kwa ajili ya serikali kutoa uamuzi nk.