Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD Logo

OCPD NA TPBA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA KITAALUMA NA MAFUNZO

Imewekwa: 11 October, 2026
OCPD NA TPBA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA KITAALUMA NA MAFUNZO

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imepokea ugeni kutoka Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA) kwa lengo la kujadili namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kitaaluma, mafunzo na kujenga uwezo wa wanachama wa Chama hicho.

Akizungumza wakati wa ugeni huo, Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD), Bw. Onorius Njole, amesema kuwa moja ya vipaumbele vya OCPD ni kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo mbalimbali ili kuongeza ujuzi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Moja ya vipaumbele vya OCPD ni kuimarisha uwezo wa kitaaluma wa watumishi wetu, hadi sasa, baadhi ya watumishi wamehitimu mafunzo katika nyanja mbalimbali, zikiwemo Uandishi wa Sheria, Sheria za Usafiri Majini na Sheria za Kodi, na baadhi ya watumishi wanaendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili katika maeneo mbalimbali ya sheria," amesema Bw. Njole.

Aidha, Bw. Njole ameeleza kuwa OCPD ina utaratibu wa kuendesha mafunzo ya Uandishi wa Sheria (Legislative Drafting) kila Jumatatu, ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ujuzi na kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa Ofisi hiyo.

"Ofisi yetu huendesha mafunzo ya Uandishi wa Sheria kila Jumatatu, na mafunzo haya yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuwajengea uwezo watumishi wetu na kwa sasa, tunaangalia namna ya kupanua wigo wa mafunzo haya ili kuwawezesha pia wanasheria kutoka taasisi nyingine kunufaika nayo," amesema Bw. Njole.

Akijibu swali la Makamu Mwenyekiti wa TPBA, Bi. Farida Kiobya, kuhusu fursa za watumishi wa OCPD kupata mafunzo kwa vitendo katika taasisi nyingine za kisheria, Bw. Njole amesema kuwa Ofisi hiyo inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) katika kuwapatia watumishi wake mafunzo hayo huku akiongeza kuwa baadhi ya watumishi wanajiandaa kushiriki mafunzo hayo, ambayo yameonekana kuwa na manufaa katika kuimarisha uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa kiutendaji.

Kwa upande wake, Rais wa TPBA, Bw. Bonaventure Mwambaja, amemshukuru Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa mapokezi mazuri na kupongeza juhudi za OCPD katika kuimarisha uwezo wa kitaaluma wa watumishi wake kupitia mafunzo endelevu.

"Tunatamani kuona baadhi ya wanachama wetu walio nje ya OCPD wakipata fursa ya kushiriki mafunzo haya ya kila wiki kupitia Chama chetu, ili nao waweze kujengewa uwezo na kuongeza ujuzi katika masuala ya Uandishi wa Sheria," amesema Bw. Mwambaja.

Ugeni huo umetoa fursa kwa OCPD na TPBA kujadili maeneo ya ushirikiano, hususan katika kubadilishana uzoefu, kuimarisha ujuzi wa kitaaluma na kupanua fursa za mafunzo kwa Mawakili wa Serikali.