Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD YAJIFUNZA FURSA ZA AI, MUSTAKABALI WA UANDISHI WA SHERIA KWENYE MKUTANO WA JUMUIYA YA MADOLA, IRELAND.

Imewekwa: 29 September, 2025
OCPD YAJIFUNZA FURSA ZA AI, MUSTAKABALI WA UANDISHI WA SHERIA KWENYE MKUTANO WA JUMUIYA YA MADOLA, IRELAND.

17-18 Septemba, 2025

Waandishi wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wameshiriki Mkutano wa Waandishi wa Sheria wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Association of Legislative Counsel – CALC), Kanda ya Ulaya, uliofanyika mjini Belfast, Ireland Kaskazini kuanzia Septemba 2025. Kupitia ushiriki huo, OCPD imejifunza kuhusu uandishi wa sheria, changamoto na fursa katika taaluma hiyo, huku mada ya matumizi ya teknolojia hususan Akili Bandia (AI) katika uandishi wa sheria ikiongoza mijadala. Aidha, mkutano huo umeiwezesha OCPD kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, kujifunza mbinu mpya na kuimarisha mahusiano na jumuiya za kimataifa katika sekta ya uandishi wa sheria.

Akizungumzia mada zilizojadiliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo, Bi. Rehema Katuga amesema Tanzania imetoa uzoefu wake kuhusu namna urasimishaji wa sera unavyorahisisha mchakato wa kutunga sheria. “Sisi kama wawakilishi kutoka Tanzania tumejadili na kutoa uzoefu wetu kuhusu  namna urasimishaji wa sera unavyochangia katika kuondoa ugumu wa kutunga sheria na nafasi ya maendeleo ya kitaaluma kwa Waandishi wa sheria katika kuhakikisha ufanisi na ubora wa kazi zao”

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora, Bw. Bavoo Junus, amebainisha kuwa mjadala mkubwa umehusu nafasi ya Akili Bandia (AI) katika uandishi wa sheria, huku washiriki wakijadili changamoto za kisheria zinazotokana na matumizi ya AI, umuhimu wa data katika kuboresha sheria, na matumizi ya mifumo ya kiteknolojia katika ofisi za waandishi wa sheria. “Kumekuwa na mjadala mpana uliohoji iwapo AI inaweza kuchukua nafasi ya binadamu katika kuandaa sheria. Tumepata uzoefu na kujifunza mengi kutoka kwa wabobezi wa sekta hiyo,” alisema Bw. Junus.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria, Bw. Shaban Kabunga, amesema wamepata uzoefu wa kipekee katika kujadili urasimishaji wa makubaliano ya kimataifa kwa kuzingatia dhana ya dualism na devolution. Ameongeza kuwa wamejifunza kuhusu namna sheria zinavyoweza kuandaliwa ili kushughulikia changamoto za kijamii, ikiwemo mifano ya sheria zinazolenga kuhalalisha makosa ya kijinsia (criminalising misogyny).

Aidha, Bw. Alfred Nyaronga, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA OCPD, ameeleza kuwa mijadala imehusu pia matumizi ya teknolojia katika kuboresha ubora wa uandishi wa sheria, ikiwa ni pamoja na nyenzo za kidijitali zinazosaidia kutathmini viwango vya uandishi.

Mkutano huo umewakutanisha Waandishi wa Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, ukiwa jukwaa muhimu la kuimarisha ubunifu, ufanisi na uhusiano wa kitaaluma katika sekta ya uandishi wa sheria.