Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MWANDISHI MKUU WA SHERIA

OCPD YASHIRIKI WARSHA YA KIMATAIFA YA UPATIKANAJI WA SHERIA ENDELEVU

Imewekwa: 18 August, 2025
OCPD YASHIRIKI WARSHA YA KIMATAIFA YA UPATIKANAJI WA SHERIA ENDELEVU

Accra, Ghana – 17 July 2025

Ofisi ya Uandishi wa Sheria na Uchapishaji (OCPD) imeshiriki katika warsha ya kimataifa kuhusu Upatikanaji Endelevu wa Sheria iliyofanyika jijini Accra, Ghana, tarehe 17 Julai 2025.

Warsha hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Spika wa Bunge la Ghana, Mheshimiwa Bernald Ahiafor, na imehusisha wadau wakuu wa sekta ya sheria wakiwemo wawakilishi wa Bunge la Ghana, Mahakama ya Ghana, Wizara ya Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Chama cha Mawakili wa Ghana, Kampuni ya Uchapishaji Ghana Ltd, na taasisi nyingine muhimu.

OCPD imewakilishwa na Bi. Rehema Katuga, Kaimu Mkurugenzi wa Urekebu wa Sheria, Mafunzo na Utafiti; Bw. Vincent Masalu, Wakili wa Serikali; na Bw. Timotheo Luambano, Mkutubi. Katika ziara hiyo, timu ya OCPD pia imetembelea Bunge la Ghana na kufanya mazungumzo na Bi. Sena, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uandishi wa Sheria.

Ushiriki wa OCPD katika warsha hiyo umechochewa na hatua kubwa iliyofikiwa na Tanzania katika kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kisheria kupitia Jukwaa la TanzLII, ambalo OCPD ni mshirika mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Kupitia jukwaa hilo, wananchi na wadau wa sheria wamekuwa wakipata nyaraka na taarifa za kisheria kwa urahisi, bure na kwa wakati.

Katika warsha hiyo, OCPD imepata fursa ya kushirikisha uzoefu wake katika usimamizi wa TanzLII, kueleza manufaa yake kwa mfumo wa sheria na jamii, changamoto zilizojitokeza, pamoja na mikakati inayotumika kuhakikisha taarifa hizo zinaendelea kupatikana kwa ufanisi. Washiriki wamejifunza mbinu mbalimbali zinazoweza kusaidia kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa sheria nchini Ghana, huku wakibainisha kuwa hatua hiyo ni msingi wa maendeleo ya kidemokrasia na kiuchumi.

OCPD imesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda, ubadilishanaji wa maarifa, na matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria kama nyenzo muhimu za kuimarisha mifumo ya kisheria barani Afrika. Aidha, imeelezwa kuwa ushirikiano wa aina hii utaendelea kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya sheria katika ukanda huu.