OCPD KUIMARISHA UPATIKANAJI WA HAKI KUPITIA MAMA SAMIA LEGAL AID
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa huduma za kisheria kwa umma kupitia ushiriki wake katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wote kwa kuwezesha wananchi kupata msaada wa kisheria kwa ukaribu na kwa wakati.
Kupitia jukwaa hili, wananchi hupata fursa ya kukutana ana kwa ana na wataalamu wa uandishi wa sheria, na hivyo kuwezeshwa kupata ufafanuzi wa kina kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria. Ushiriki wa OCPD unalenga, pamoja na mambo mengine, kutoa elimu ya umma kuhusu majukumu yake makuu ambayo ni Uandishi wa Sheria, Urekebu wa Sheria na Ufasili wa Sheria, kwa namna inayozingatia uelewa wa wadau mbalimbali.
Katika eneo la uandishi wa sheria, wananchi hufahamishwa kuhusu mchakato mzima wa kutunga sheria, kuanzia hatua ya sera hadi kuandaliwa kwa rasimu na hatimaye kuwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.
Aidha, OCPD hueleza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika hatua mbalimbali za mchakato huo, hususan katika utoaji wa maoni, ili kuhakikisha sheria zinazotungwa zinakidhi mahitaji halisi ya jamii.
Kuhusu urekebu wa sheria, wananchi hupewa ufafanuzi juu ya namna sheria zinavyopitiwa upya kwa lengo la kuziboresha bila kubadili dhamira yake ya msingi. Hii inahusisha kujumlisha marekebisho yote yaliyofanywa katika sheria husika ili kuifanya isomeke kwa pamoja kwa urahisi, kuondoa masharti yaliyopitwa na wakati, pamoja na kuoanisha istilahi na mabadiliko ya kisera na kijamii.
Katika nyanja ya ufasili wa sheria, OCPD hutoa mwongozo kuhusu tafsiri ya sheria, hususan kwa kuhamisha maudhui kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na kinyume chake, bila kupoteza maana iliyokusudiwa. Hatua hii ni muhimu katika kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi wengi zaidi na hivyo kuwezesha matumizi sahihi ya sheria katika maisha ya kila siku.
Aidha, wataalamu wa OCPD hutumia fursa hiyo kuwaelekeza wananchi namna ambavyo huduma hizi zinagusa maisha yao ya kila siku, ikiwemo umuhimu wa sheria zilizo wazi, zinazoeleweka na zinazozingatia misingi ya haki na usawa. Wananchi huhamasishwa kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisheria, jambo linalochangia kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika jamii.
Kwa ujumla, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kutoa elimu ya kisheria kwa umma bila gharama, kuongeza uelewa wa michakato ya utungaji na urekebu wa sheria, na kuwezesha ushiriki mpana wa wananchi katika masuala ya kisheria. Hatua hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha upatikanaji wa haki na kujenga jamii yenye uelewa na ushiriki hai katika mfumo wa sheria nchini.
